Mwisho wa miaka 1000 Kristo anarudi duniani akifuatana na
waliokombolewa na jeshi la malaika. Anawaita waovu waliokufa waamke ili wapate
malipo yao ya ajali. Wanatokea wengi sana wasiohesabika, kama mchanga wa pwani
wakiwa na hali zao za maradhi na kifo. Tofauti kubwa na wale waliofufuliwa mara
ya kwanza.
Kila jicho linamwangalia Mwana wa Mungu jinsi alivyo
mtukufu. Waovu wanapaza sauti kwa umoja wakisema, “Amebarikiwa ajaye kwa jina
la Bwana”. Mathayo 23:39. Hasemi hivyo kwa upendo, ila tu ukweli wa mambo
unawalazimisha kusema hivyo bila kutaka. Jinsi waovu walivyokufa wakiwa na hali
ya ukafiri, ndivyo watafufuka wakiwa na hali hiyo. Hakuna nafasi ya kurekebisha
tabia zao.
Nabii asema, “Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima
wa Mizietuni …. Nao mlima wa mizeituni utapasuka katikati yake” Zekaria 14:4.
Mji wa Yerusalemu unaposhuka chini, kutoka mbinguni, utatua juu ya mahali
palipotayarishwa na Kristo pamoja na watu wake na jeshi la malaika, wanaingia
mjini.
Wakati shetani alipofungwa asipate mtu wa kudanganya alikuwa
katika hali mbaya sana, lakini sasa aonapo waovu wamefufuka jeshi kubwa,
matumaini yake yanamrudia. Anakusudia kuendelea na mapambano tu, wala asisalimu
amri. Atalipanga jeshi lake vema, maana wote hao ni waasi kama yeye, wako
tayari kufanya kama apendavyo. Hajitaji kuwa yeye ni shetani, bali ajitaja kuwa
mtawala wa ulimwengu kihalali. Anatumia hila zake ili kuwahadaa. Kwamba ni yeye
mrithi wa ufalme ila ananyang'anywa haki yake kwa dhuluma. Anajidai kuwa yeye
ni mkombozi, anao uwezo wa kushinda vita, kwamba uwezo wake ndio umewatoa makaburini.
Shetani anawatia nguvu wote walio dhaifu, na kuwachochea kwa bidii ili
wakauteke mji wa Mungu. Anaona jeshi kubwa la watu waliofufuka na kusema kuwa
yeye kama kiongozi wao atashinda na kutwaa enzi yake.
Katika jeshi hilo yamo majitu ya zamani yaliyoishi kabla ya
gharika, majitu makubwa yenye akili na uwezo mwingi kimawazo, ambao walikuwa
waasi waliosababisha gharika. Pia kulikuwamo na wafalme na majemadari wakuu
ambao siku zao hawakushindwa vita kamwe. Watu hawa hawakubadilika, maana katika
kifo hakuna kubadilika. Walipofufuka walikuja na hali yao ile ya vita na
ukatili.