Katika shule za masinagogi, wanafunzi wakiwa chini ya
waalimu wa Kiyahudi, walifundishwa kushika kawaida zisizokuwa na hesabu kwa
wingi, ambazo kuhesabiwa kuwa ndizo za dini kamili, zenye kuonyesha kuwa watu
hawa ni washika dini hasa. Lakini Yesu hakushughulika na mambo kama hayo. Tangu
utoto wake, Yesu hakuhangaika na kawaida hizo. Maandiko matakatifu ndiyo
yalikuwa masomo yake ya kawaida, na maneno, “Ndiyo asemavyo Bwana”, ndiyo
yalikuwa kinywani mwake daima.
Aliona kuwa watu walikuwa wakijitenga na neno la Mungu, ila
tu wakishika kawaida ambazo hazina faida yoyote. Katika huduma zao ambazo si za
imani, hazikuwaletea utulivu rohoni mwao. Hawakujua uhuru wa roho unaoletwa na
neno la Mungu linapoaminiwa. Ingawa Yesu hakukubaliana na halli hiyo kuchanganya
neno la Mungu, na hadithi za kibinadamu, walakini hakuwashambulia walimu hao,
wala kawaida zao. Walipomlaumu kwa hali yake tofauti na wao, alileta neno la
Mungu kuwa ndiyo msimamo wake.
Yesu alijaribu kuwapendeza wale aliokutana nao. Kwa kuwa
alikuwa mtu mwungwana sana, waandishi na wazee walidhani kuwa ataweza kugeuzwa
upesi na kufuata kawaida zao. Lakini aliwauliza mahali wanaposoma katika
maandiko, mambo hayo. Yeye alitii kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu,
lakini hadithi za wanadamu hakuzijali. Yesu alionekana kujua Maandiko kutoka
mwanzo mpaka mwisho, naye aliyatumia katika ukweli wake. Walimu wa Kiyahudi,
yaani walimu wakuu, walijidai kuwa wao ndio wawezao kuyafafanua Maandiko katika
ukweli wake. Walijua kuwa wasingeweza kupata neno katika mandiko liwezalo
kukubaliana na mambo yao. Hata hivyo walichukizwa kwa sababu Yesu alipingana
nao. Walipokosa kumvuta Yesu, waliwaambia wazazi wake kuhusu ukaidi wa mtoto
wao, hivyo Yesu akakabiliwa na magombezo ya Yusufu na Mariamu.
Tangu utoto wake, Yesu alianza kujitegemea na kujenga tabia
yake. Kulitii Neno la Mungu, kulikuwa jambo muhimu kwake, kuliko neno lolote,
hata upendo kwa wazazi wake haukuweza kumgeuza, asitii Neno la Mungu. Lakini
hali ya walimu wakuu kulimsikitisha sana, akawa na huzuni katika maisha yake,
Alijifunza fundisho gumu la kukaa kimya na kuvumilia sana.
Ndugu zake, yaani wana wa Yusufu waliungana na walimu wa
Kiyahudi. Waliyaheshimu mapokeo ya wanadamu zaidi kuliko neno la Mungu, na
walimlaumu Yesu kuwa ni mkaidi. Lakini ujuzi wake uliwashangaza marabi kwa
jinsi alivyokuwa na majibu yake. Walakini hawakujifunza kuwa alikuwa
akiwafundisha. Walitambua kuwa aliwazidi katika ujuzi, wala hawakuelewa kuwa
asili ya ujuzi wake ni wapi.