Watu wengi huona kazi za mwovu, zenye matokeo ya maafa na
taabu za kila aina. Swali linachipuka vichwani kwamba inawezekanaje mambo kuwa
hivyo chini ya Mungu mwenye hekima yote, uwezo wote, na upendo wote. Watu
wanaopata kuwa na mawazo ya jinsi hii hujipatia udhuru wa kuukana ukweli wa
maandiko matakatifu. Mapokeo na kulitafsiri vibaya neno la Mungu kuhusu tabia
ya Mungu ilivyo, na asili au msingi wa serikali yake, na kanuni zake za
kushughulikia dhambi huwatia watu gizani na mashakani.
Haiwezekani kueleza asili ya dhambi ili kufahamu mwanzo wake
na jinsi ilivyo. Walakini kuna maelezo ya kutosha kufahamu mambo ya dhambi na
mwisho wa dhambi pia, ili kudhihirisha ukarimu na haki ya Mungu. Mungu hakuwa
ndiye asili ya dhambi. Kwa Mungu hakuna hali ya machafuko, wala unyimivu wa
neema yake, wala upungufu wowote katika serikali yake, ambao unaweza
kusababisha uasi na machafuko. Dhambi ni mwingilio wa uasi bila kutakiwa, na
hakuna awezaye kuelezea. Kuitetea ni kule kuikubali. Kama isingelitetewa,
isingalikuwapo kabisa. Dhambi ni uhasama kati yake na sheria ya upendo, ambayo
ndiyo msingi wa serikali ya Mungu.
Kabla dhambi haijaingia duniani, kulikuwa na amani na furaha
kote katika malimwengu. Kumpenda Mungu kulikuwa jambo kuu kabisa, na upendo
kati ya viumbe ulikuwa hausemeki, Kristo, ambaye ni Mwana wa pekee alikuwa
pamoja na Baba wa milele, katika asili, tabia na makusudi. Ni yeye tuliyeingia
katika mashauri yote ya Mungu, na makusudi ya Mungu. “Kwa kuwa katika yeye vitu
vyote viliumbwa vilivyo mbinguni …. Ikiwa ni vitu vya enzi, na usultani, au
enzi, au mamlaka.” Kol. 1:16.
Sheria ya upendo ndiyo iliyokuwa msingi wa serikali ya
Mungu. Furaha na raha ya viumbe vyote vilivyoumbwa ilitegemea jinsi
walivyoafikiana na kanuni za haki. Mungu hana furaha na kulazimisha viumbe
wamtii. Kwa viumbe vyote alitoa uhuru kamili, uhuru wa dhamiri ili wamtumikie
kwa uhuru kila mmoja kwa hiari yake, siyo kwa shuruti.
Lakini alikuwako mmoja aliyechafua mpango huu wa uhuru.
Dhambi ilianzia kwake ambaye ndiye aliyekuwa wa pili kwa Kristo, mwenye heshima
kuu mbele za Mungu. Kabla hajaanguka, Lusifa alikuwa “Kerubi wa kwanza afunikwaye”
mtakatifu, asiye na waa. Bwana Mungu asema hivi: “Wewe wakitia muhuri kipimo
umejaa hekima na ukamilifu wa uzuri. Ulikuwa ndani ya Edeni, bustani ya Mungu;
kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako…. Wewe ulikuwa kerubi mwenye
kutiwa mafuta afunikaye, nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa
Mungu, umetembea huko na huo kati ya mawe ya moto ulikuwa mkamilifu katika njia
zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako…. Moyo wako
uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya
mwangaza wako; Umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu” “Nawe ulisema nitakiinua
kiti changu juu kuliko nyota za Mungu….. nami nitaketi katika mlima wa mkutano
…. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana na yeye aliye juu” Eze.
28:12-17; 28:6; Isaya 14:13-14.
Heshima ya kufunika ambayo Baba aliitoa kwa mwanawe
ilitamaniwa na malaika huyu, ingawa alikuwa na heshima. Heshima ya Kristo,
ilimhusu yeye tu, wala si mwingine. Basi sasa alama ya kutoridhika ilionekana
katika umoja wa ajabu uliokuwa mbinguni. Kujitukuza kwa ubinafsi hakukuruhusiwa
huko. Lilikuwa chukizo baya mno kufikiri. Utukufu wa Mungu ulikuwa unatosha
kabisa. Baraza la mbinguni lilimsihi juu ya nia yake, kuwa aiache. Mwana wa
Mungu alimweleza uzuri na haki ya mwumbaji, pamoja na utakatifu wa sheria yake.
Kama akijitenga na sheria hiyo, Lusifa atakuwa amemdharau Mwumbaji wake, na
kujiletea uharibifu mwenyewe. Lakini onyo hilo lilipingwa. Lusifa aliendelea
kumwonea Kristo wivu.
Kiburi kiliongeza tamaa ya ukuu wa Lusifa, akawa mtaka
makuu. Heshima kuu aliyopewa haikumfanya awe na shukrani, kwa Muumba wake.
Alikaza nia yake ya kufanana na Mungu. Walakini mwana wa Mungu peke yake ndiye
alikuwa na cheo hicho, yaani yeye alikuwa katika umoja na Baba kwa kila hali
katika mashauri yote ya Mungu Kristo alishiriki. Lakini Lusifa hakuwa na hadhi
hiyo. Hivyo aliuliza kwa nini Kristo tu awe na hadhi hiyo na mimi sivyo?