MJUE SANA MUNGU,ILI UWE NA AMANI, NDIVYO MEMA YATAKAVYOKUIJIA

Tusk aitaka Ujerumani kuilinda mipaka ya EU

Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk ameitaka Ujerumani kuchukua hatua za ziada kuilinda mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya ili kukabiliana na mzozo wa wahamiaji unaolikumba bara hilo.




Rais huyo wa baraza la Umoja wa Ulaya amenukuliwa na gazeti la Ujerumani Welt Am Sonntag akisema kuwa Ujerumani huenda ikahitajika kutekeleza wajibu wake wa uongozi katika kuhakikisha mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya inalindwa kikamilifu.
Ujumbe wa Tusk kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ni kuwa mahitaji ya kiusalama ya Umoja wa Ulaya huenda yakawa tofauti na ya Ujerumani.
Ujerumani ina wajibu kwa EU
Tusk ameongeza kusema kuwa anaelewa iwapo Ujerumani kutokana sababu za kihistoria ikawa na ugumu katika kutekeleza sheria kali katika mipaka yake lakini uongozi wa Ujerumani una jukumu kuambatana na sheria za Umoja wa Ulaya kuilinda mipaka ya nje vilivyo kuambatana na taratibu za mshikamano wa nchi wanachama wa Umoja huo.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Tusk ambaye ni Waziri mkuu wa zamani wa Poland, hata hivyo ameisifu serikali ya Ujerumani kwa kuwa tayari kuwapokea maelfu ya wahamiaji na kuitaja hatua hiyo ya Ujerumani kuwa kielelezo bora zaidi cha ukarimu na ustahimilivu katika historia ya bara Ulaya.
Rais huyo wa baraza la Umoja wa Ulaya anatarajiwa kufanya mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo jioni mjini Berlin, huku akikabiliwa na shinikizo kutoka nchi za mashariki mwa Ulaya kuchukua hatua zaidi za kuhakikisha mipaka inalindwa zaidi, kuliko kuangazia zaidi namna ya kuwapokea wakimbizi wapya.
Ujerumani imewapokea wahamiaji 758,000 kati ya mwezi Januari na Oktoba mwaka huu na kusababisha Merkel kushutumiwa ndani ya nchi kwa sera yake ya kuwapokea wakimbizi.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana kwa mkutano wa tano wa kilele kuujadili mzozo huo wa wahamiaji siku ya Alhamisi, siku moja baada ya mkutano mwingine kati ya Umoja huo na nchi za Afrika utakaofanyika Malta siku ya Jumatano kujadili suala hilo la wahamiaji.
Mzigo wa wakimbizi usambazwe
Ajenda kuu ya mkutano wa Alhamisi itakuwa ni utekelezwaji wa mpango wa kusambaza wakimbizi 160,000 miongoni mwa nchi wanachama wa umoja wa Ulaya, kuimarisha ushirikiano na Uturuki na kuanzishwa kwa vituo vya muda vya kushughulikia kwa haraka maombi ya hifadhi mipakani.
Wakimbizi kutoka Syria wakiwasili Ujerumani
Wakimbizi kutoka Syria wakiwasili Ujerumani
Mipaka ya bara Ulaya inaonekana kuwa wazi mno huku maelfu ya wahamiaji wakiingia barani humo kupitia bahari za Aegean na Mediterania. Wakati huo huo kituo cha televisheni cha Uingereza cha Channel 4 siku ya Jumamosi kiliripoti kuongezeka kwa idadi ya wahamiaji wanaojaribu kufikia kisiwa cha Ugiriki cha Lesbos kabla ya msimu wa baridi kali kuanza.




Subscribe to receive free email updates: