MJUE SANA MUNGU,ILI UWE NA AMANI, NDIVYO MEMA YATAKAVYOKUIJIA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi yatoa idadi ya Wabunge wa Viti Maalum .....CCM viti 64 CHADEMA viti 36 CUF viti 10

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Mhe. Damian Lubuva ametangaza idadi ya wabunge wa Viti Maalum leo katika ukumbi wa ofisi za Tume hiyo jijini Dar es Salaam.
 
Jaji Lubuva akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari alisema kwamba, kwa mujibu wa Ibara ya 66(1) (b) na Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, Tume imepewa mamlaka ya kutangaza Viti Maalum vya wabunge wanawake visivyopungua asilimia 30 ya wabunge. Idadi ya Viti Maalum iliongezeka na kufikia asilimia 40 mwaka 2010 kwa mujibu wa uamuzi wa Serikali.
 
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 viti maalum idadi yake ni 113, kutokana na kuwepo majimbo 8 ambayo hayakufanya uchaguzi mgawanyo wa Viti Maalum kwa sasa ni 110, viti 3 vilivyobaki, vitagawanywa baada ya kufanyika kwa uchaguzi katika majimbo hayo.”Alisema Jaji Lubuva.
 
Jaji Lubuva alisema kuwa, vyama ambavyo vimekidhi vigezo vya kikatiba na kisheria na kupata angalau asilimia 5 ya kura zote halali za wabunge ndio vitakavyo kuwa na wabunge wa Viti Maalum. Huku idadi ya wabunge Viti Maalum kutoka katika vyama vinategemea na idadi ya kura halali za wabunge ambavyo vyama hivyo vimepata.
 
Kutokana na matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini mwishoni mwa mwezi Oktoba, idadi ya kura halali ya wabunge kwa vyama vitatu vilivyopata angalau asilimia 5 ni CCM kura 8,333,953 imepata jumla ya Viti Maalum 64, CHADEMA kura 4,627,923 imepata jumla ya Viti Maalum 36 na CUF kura 1,257,051 imepata jumla ya Viti Maalum 10.
 
Majina ya Wabunge wa Viti Maalum yatapatikana katika vyama husika kwa mujibu wa orodha iliyowasilishwa Tume na kila chama. 

Subscribe to receive free email updates: