MJUE SANA MUNGU,ILI UWE NA AMANI, NDIVYO MEMA YATAKAVYOKUIJIA

SHERIA ZILIZOISHIA MSALABANI

Somo hili ni la maana sana kujifunza kwa ajili ya wokovu wetu, shetani amejaribu kulitumia somo hili kama mtego wa kuwanasa watu hasa wale ambao hawana muda wa kukaa na kutafakari kwa undani neon la Mungu, wakitegemea maelezo ya viongozi wao wa dini au madhehebu.
Kuna mafungu mengi katika Biblia yanayoeleza kuwa kuna sheria zilizoishia msalabani, ambazo zilikuwa kivuli cha mambo yaliyokuwa yanatazamiwa. Mtume Paulo anasema Sheria ikishikwa sasa Kristo si Mwokozi wetu kwa sababu tunategemea sheria iliyokufa [Wagalatia 5:4-6, 4:1-11]. Hivyo wengi hawaelewi, na kuna maswali mengi kuhusu sheria zilizokufa baada ya Kristo kufa msalabani, kwa sababu Biblia kwa upande mwingine inasisitiza juu ya ulazima wa kutii na kushika Amri za Mungu kwa yeyote aliyeokolewa. Soma: 1Yohana2:4 “Asemaye nimemjua wala hashiki Amri ni muongo wala kweli haimo ndani yake”, Mithali 28:9, Ufunuo 14:12, Marko 7:6-8, Mathayo 5:17-19   n.k..

Katika Biblia Sheria zimegawanywa katika makundi makuu mawili na zinaitwa Sheria za Mungu na Sheria za Musa. Kabla hatujaelezea ni kwa namna gani zinategemeana, yafuatayo ni maelezo yanayotoa tofauti kati ya hayo makundi mawili.


SHERIA YA MUNGU
1.  Iliandikwa na Mungu Mwenyewe 
     (Kutoka 31:18)
SHERIA ZA MUSA [TORATI]
1.  Iliandikwa na Musa
     (Kutoka 31:9)
2.  Iliandikwa juu ya Mawe
     (Kumbukumbu 10:1-4, 9:10 )
2.  Iliandikwa ndani ya Gombo au Kitabu
     (Kumbukumbu 31:24)
3.   Ilitunzwa ndani ya Sanduku la Agano
      (Kumbukumbu 10:5)
3.  Ilitunzwa Nje ya sanduku la Agano
     (Kumbukumbu 31:26)
4.  Huitwa Sheria ya Mungu
     (Zaburi 1:2, 11:1)
4   Huitwa Sheria ya Musa
     (Malaki 4:4, Mathayo 15:5)
5.  Ni za Milele na ni Kamilifu
     (Zaburi 111:7-8, Mathayo 5:17-19, Zaburi 19:7)
5.  Baadhi ziliondolewa na sio kamilifu
     (Ebrania 9:10-11, 7:1, Efeso 2:15)
6.  Ni Takatifu, ya Haki na Njema
     (Warumi 7:12)
6.  Baadhi zilikuwa kivuli cha Kifo cha Yesu Kristo
     (Ebrania 10:1, 7:12) – Iliishia msalabani
7.  Jumla ziko kumi
     (Kumbukumbu 4:12-13)
7.  Ziko nyingi (Huitwa chuo)
      (Kumbukumbu 31:24-26, 2Nyakati 35:12)
8.  Ndiyo Jumla na Muhtasali wa Mapenzi ya Mungu,  Ndiyo
     huonyesha Dhambi ni nini.
     (Mhubiri 12:13, Rumi 2:13, Yakobo 2:10:12,
      Rumi 7:7, 3:20)

8.   Kwa wakati wake zilimsaidia mtu kuhesabiwa haki  na
       kuwafanya wengi waogope kutenda dhambi au kuvunja
      Amri za Mungu. Mfano. Sheria za Kafara.



Kiini cha kuwepo Sheria za Musa, na Kristo kuja kutufia msalabani ni Dhambi (Uasi wa Sheria za Mungu).  Amri kumi zikiondolewa hakutakuwa na Dhambi, hivyo hakutakuwa na hukumu, na hatimaye hakutakuwa na haja ya kuwepo Mwokozi, na tendo la msalaba litakuwa bure. Shetani ametumia mbinu ya kuzichanganya sheria hizi mbili na  amefaulu kuwateka mamilioni ya watu wa Mungu bila ya wao kujua. Sheria au Amri za Mungu ndicho kipimo cha wokovu na utiifu wetu kwa Mungu, wala haziwezi kubadilika kwa maana YEYE NI MKAMILIFU NA SHERIA ZAKE NI KAMILIFU WALA HANA KIGEUGEU [Isaya 8:20, Mithali 28:9, Yohana 14:15, 15:10, 8:29].

Amri za Mungu kama zilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu mwenyewe katika mbao mbili za mawe, ndizo jumla ya mapenzi ya Mungu, na ndicho kioo kinachotuonyesha kuwa tuko safi au wachafu. Shetani leo amefaulu kuwaongoza wengi kuzichukia Sheria za Mungu wala hawataki kuzisikia. Amri za Mungu zinapatikana katika Kutoka 20:1-17,  Hebu chukua Biblia yako na usome  mistari hiyo, kasha linganisha na jinsi ulivyofundishwa Amri za Mungu au linganisha jinsi zilivyoandikwa kwenye vitabu vya mafundisho. Mfano: Katekisimo ya Kanisa lako. Kama utakuta kuna tofauti basi fanya maamuzi ya kufuata Neno la Mungu kama Yesu alivyotoa wito katika Injili ya  Marko 7:6-8. Kuendelea kushika Mapokeo au mafundisho ya wanadamu na kuziacha Amri za Mungu ni kuchagua kupotea milele, na Ibada yako itakuwa ya Bure kama Kristo alivyotoa tahadhari.

MAELEZO JUU YA SHERIA ZILIZOISHIA MSALABANI

1. SHERIA ZA KUTOA KAFARA [ UPATANISHO AU ONDOLEO LA DHAMBI
Tangu mwanzo Mungu alimwambia mwanadamu kuwa akiasi maagizo hakika atakufa Mwanzo 2:16-17, hata hivyo kwa rehema zake akaandaa mpango wa wokovu kwa Mwanadamu aliyeanguka dhambini, mpango ulikuwa ni kumtoa mwane Yesu Kristo afe badala ya Mtu aliyeasi. Kabla ya Kristo kufa msalabani Mungu aliweka taratibu zingine ambazo zilikuwa badala ya Kafara halisi ya Kristo. Mwanzoni alitoa Sheria ya Tohara na baadaye Mungu aliruhusu Wanyama watolewe kafara ikiwa ni kivuli cha kafara halisi ya Kristo. (Walawi 4:27-29, 17:11, 16:5-30, Ebrania 9:7). Siku maalumu za kufanya huduma hizo, ziliitwa Sabato au Pumziko takatifu kwa ajili ya Upatanisho (Walawi 23:26-32, 25:8-10), pia kulikuwa na sikukuu za miandamo ya miezi zilizofuatia siku hizo za Upatanisho (Hosea 2:11).

Sikukuu hizo za upatanisho pamoja na Kafara vilikuwa kivuli cha Kafara halisi ya Kristo, hivyo vilikoma baada tu Yesu Kristo kufa pale Msalabani. Waebrania 9:25-26. Baada ya hapo wote tunaokolewa kwa neema ya Kristo iliyotokana na Kafara yake iliyotolewa mara moja pale Kalvari.

2. SHERIA ZA KIJAMII
Sheria hizi zinaitwa za kijamii kwa sababu zilitumika kulinda amani katika jamii, na kuwafanya watu waogope kufanya uovu (Watii sheria za Mungu).  Adhabu kali zilitolewa kwa yeyote anayevunja Amri za Mungu  Mfano: Kuwapiga mawe wazinzi hadi kufa. Watu waliogopa kutenda uovu kwa sababu ya adhabu sio kwamba walimheshimu Mungu ndani ya mioyo yao.

Baada ya Kristo kufa msalabani, wale wote wanaofungua mioyo yao na kumpokea Yesu Kristo kwa Imani, wanapokea Uweza wa kushinda dhambi.  Uweza wa Mungu hujenga asili ya kuchukia dhambi ndani ya Moyo wa Mwanadamu. Hivyo sheria za kumuogopesha mtu asifanye dhambi wakati Moyo wake unapenda au kutamani dhambi hazina kazi. Hiki ndicho kipimo cha Mkristo aliyezaliwa mara ya Pili. Yeyote mwenye Moyo wa Kutamani dhambi, hata kama inashindikana kutekelezwa, Mungu anamhesabia dhambi Matahayo 5:27-28, kwa sababu ni wazi mtawala wa Moyo ni Shetani sio Roho Mtakatifu.

3. SHERIA ZA AFYA
Ni sheria ambazo Mungu alizitoa kwa ajili ya kulinda Afya za watoto wake, alitoa maelekezo juu ya Vyakula vinavyofaa kuliwa na visivyofaa, hii ilikuwa kwa ajili ya Afya. Kwa maelezo zaidi juu ya somo hili la AFYA, nimeandaa somo maalumu linaloezea uhusiano uliopo juu ya Afya zetu na Wokovu.

WOKOVU NA SHERIA
Fundisho la Biblia kuhusu sheria zote mbili juu ya wokovu ni kama ifuatavyo:

1.    Wale wote waliompokea Kristo hawako chini ya Sheria za Makafara, wako huru Kabisa.

2.    Baada ya Kristo kuja, hakuna sheria za adhabu za kijamii – mf. Kupiga mawe wazinzi n.k.

3.   Sheria za Mungu [Amri Kumi] hazimuokoi Mtu, zenyewe zipo kama kioo kinachoonyesha uchafu lakini haziwezi kukusafisha, ili uchafu utoke ni lazima uchukue Maji unawe. Maji ni Damu ya Kristo ambayo kwa Imani tunatakaswa kwayo. Kutunza au kutii sheria ni matokeo ya kuokolewa, ni yule tu aliye chini ya Neema ya Kristo, ndiye anayeweza kutii mapenzi ya Mungu.

NB: Hatuhesabiwi haki kwa sababu tunashika Sheria za Mungu, bali tunahesabiwa haki kwa sababu NEEMA YA YESU KRISTO imetupatia ushindi wa Dhambi na kutufanya tuwe safi pasipo mawaa mbele za Mungu. Kujitahidi kutii Amri za Mungu kwa Nguvu zetu, kutaka kuhesabiwa haki kwa matendo ya Sheria, kitu ambacho hakiwezekani.

 Kitu cha kushangaza ni pale wengi wanadai wameokolewa huku wakiendelea kuvunja au kutotii baadhi ya Amri za Mungu kwa kusingizia kuwa chini ya Neema.Tito 2:11-12, Inatueleza kazi ya neema, Yesu hakufa msalabani ili baadhi ya dhambi zihalalishwe, alikuja ili kile kilichoshindikana kwa mwili kiwezekane kwa uwezo wa Roho mtakatifu, kwa ajili ya kutukamilisha tuonekane bila mawaa mbele za Mungu wakati wa Hukumu. Na kama tunakiri kuwepo kwa hukumu ya haki, basi ni lazima tujue kuwa kuna vigezo ambavyo vitatumika kuhukumu ambavyo Mungu anasema ni Amri zake.

Subscribe to receive free email updates: