JE?; KUNA MAISHA BAADA YA KIFO?
by charles shibita
Kuna mafundisho mengi tofauti juu ya Mtu anapokufa, wengine wanasema anaenda kuzimu, wengine jehanamu, wengine peponi, wengine haendi kokote. Je Mungu anasemaje ?, jibu la kweli tunalipata kutoka katika Neno la Mungu kama lilivyochambuliwa kwenye vipengele vifuatavyo.
(1) MTU AU NAFSI HAI
Mtu au Nafsi HAI ni muungano wa vitu viwili MAVUMBI na PUMZI YA MUNGU, ( Mwanzo 2:7, Ezekiel 18:4 Isaya 53:12 ), Au NAFSI HAI = MAVUMBI + PUMZI YA MUNGU. Hivyo, vitu hivi viwili vikitengana hamna nafsi HAI na ndicho huitwa kifo, mtu anakuwa kuzimu.
(2) KUZIMU KUNA NINI ?
Maandiko yanasema KUZIMU ni sehemu penye ukimya, Mtu aliyekufa au aliyekuzimu hawi na Ufahamu, hivyo hajui lolote juu Mbinguni na Duniani. ( Mwanzo 3:19, Mhubiri 3:18-20, Mhubiri 9:5-6, Zaburi 104:29 ). Pumzi inayomrudia Mungu sio nafsi hai, hivyo inakuwa sawasawa tu na kabla ya mtu hajazaliwa au kuumbwa.
(3) WAKRISTO HALISI HUKIITA KIFO KUWA NI NINI ?
Neno la Mungu linasema kifo ni sawa na USINGIZI, Daudi alikiita kifo kuwa ni USINGIZI WA MAUTI. Kama mtu asivyojua lolote akiwa usingizini ndivyo Marehemu anavyokuwa kabulini hadi kristo atakapokuja. ( Daniel 12:2, Yohana 11:11, Mathayo 27:52, 1Thesalonike4:13, Ayubu 17:13, Luka 8:52-53, Zaburi 13:3, 1Korintho 15:20-23 ).
(4) KUNA UHUSIANO WOWOTE KATI YA WALIOKUFA NA MUNGU ?
Mungu hana uhusiano wowote na waliokufa, kwa sababu hawana kumbukumbu lolote, Pia Kristo alisema Mungu sio wa waliokufa. ( Mathayo22:32, Zaburi 146:1-4 ). Hivyo watakatifu wote waliokufa hawako Mbinguni wamelala kabulini.
(4) NI LINI WATAKATIFU WALIOKUFA WATAONANA NA MUNGU ?
Mbinguni au Peponi wanaenda watu hai au ( NAFSI HAI) wakivishwa miili ya Mbinguni ( Mfano: Eliya, Henoko, Kristo nk. ), Kristo kama alivyotuahidi atakuja kutuchukua pamoja na waliokufa atakapokuja mara ya pili. Tutarudishiwa Pumzi na kuwa hai tena, ndipo tutavishwa miili ya mbiguni na kuanza safari ya kwenda kwa Baba yetu Mbinguni. ( Yohana 5:28-29, 1Thesalonike 4:15-17, Yohana 14:1-3, 1Korintho 15:51-52, Ayubu 14:12, Matendo 24:15, Matendo 2:34 ). Yesu mwenyewe alipokufa msalabani na kuzikwa hakuenda mbinguni hadi alipofufuka ( Yohana 20:17 )
(5) LINI WAOVU WATAINGIA JEHANAMU ?
Waovu wataingia Jehanamu baada ya Kristo kupitisha hukumu, Ni ahadi ya kristo pia kuja siku ya mwisho kuuhukumu ulimwengu na kutoa adhabu ya Moto. Waovu watafufuliwa katika ufufuo wa pili, wote watakuwa hai na kudhihirishiwa matendo yao yote, ndipo MOTO utawashwa kwa ajili yao. ( Ufunuo 6:14-17, 20:13-15, 22:12, Mathayo 16:27, 2Petro3:7-10, Isaya 25:9, Yohana 5:28-29, Mathayo 25:31-41, Malaki 4:1, Rumi 2:5-6 ).
Viongozi wa dini wanaofundisha kuwa Mtu akifa hapohapo anaenda Jehanammu (Motoni) au Peponi (Mbinguni) ni lazima tuwaangalie sana huenda kwa kujua au kutokujua wanatumiwa na yule adui kwa hila kuvuruga ukweli halisi juu ya mpango wa Mungu Kuuhukumu ulimwengu kwa haki kama Injili inavyosema.
MAFUNGU YA BIBLIA YANAYOTUMIWA KUPOTOSHA UKWELI
WAEBRANIA 9:27.
Kama tulivyosoma hapo juu baada ya Kifo hakuna kinachoendelea, yaani mtu hana nafasi tena ya kuamua kufanya mema au mabaya. Kilichoandikwa kitabuni mbinguni dakika ya mwisho ya kukata Roho, ndicho kinapelekwa hukumuni siku ya mwisho Kristo atakapokuja. Mtu akifa rekodi za matendo yake zinafungwa tayari kwa hukumu. Pia neno la Mungu linasema hukumu kwa waliokufa imeshaanza, hii inaitwa hukumu ya upelelezi ambapo vitabu vya kumbukumbu kwa waliokufa vinapitiwa mmoja baada mwingine hadi siku ya Mwisho.
LUKA 23:39-43.
Hapa Kristo alikuwa anamhakikishia mhalifu kuwa watakuwa wote peponi, Neno halijasema "LEO HII" Kristo amesema "LEO HIVI". Hapo kuna makosa ya uchapaji na tafsiri kutoka lugha ya awali ya kigiriki, alama ya koma (,) kwa kiswahili sahihi haijawa mahali pake. Hata hivyo kama tulivyosoma Kristo alithibitisha kuwa hakuenda Mbinguni (Peponi) alipokufa ( Yohana 20:17, Yohana 14:1-3 ). Pia ukumbuke kuwa Mungu sio kigeugeu na neno lake halipingani.
LUKA 16:19-28.
Mfano huu wa Tajiri na Maskini Lazaro, umekuwa ni kigezo kikubwa cha Shetani kutumia kuwavuruga watu washindwe kuielewa Injili na ahadi za Kristo. Kabla ya kutoa maelezo juu ya mfano huo soma na kutafakari mifano mingine iliyotolewa na Kristo ( mfano: Luka 16:1-15 ) Je unaweza kusema "Kristo alihalalisha mali ya Udhalimu ? ", Mifano iliyotolewa kwenye Biblia, kabla hatujaichukuwa kama mafundisho, ni lazima tuangalie vitu vufuatavyo : Mfano ulitolewa na nani, Kwa watu wa aina au hali au Tabia gani, Dhumuni au Fundisho maalumu la mfano, na Je biblia nzima inasemaje juu ya Fundisho hilo.
Katika mfano huo Fundisho au Dhumuni lilikuwa juu ya hali halisi ya Matajiri wenye Ubinafsi na Maskini, itakavyokuwa wakati Kristo atakapokuwa akimlipa kila mtu mshahara wake. Kristo hakuwa na maana kuwa mtu akifa anakwenda Peponi au Jehanamu halafu wanakuwa wanawasiliana. Shetani anajua kuchanganya ukweli na uongo lakini kwa kuichambua biblia nzima kwa msaada wa Roho mtakatifu, siri zote za muovu zinafichuliwa. Watu wengi leo wamechanganyikiwa hadi wanasema biblia inajipinga.
MAFANIKIO YA SHETANI KUPITIA SOMO ZIMA LA WAFU
[A]
Shetani amefanikiwa kueneza uongo wake aliousema kwa mama yetu EVA katika Bustani ya Edeni. Mungu alisema "hakika mtakufa", Shetani alisema "hakika hamtakufa". Hata hivyo Mungu kwa njia ya manabii, Kristo na Mitume amezidi kuthibitisha kuwa Binadamu sharti afe, Kufa ni Amri tangia Edeni. Na shetani anaendeleze uongo kuwa Mtu hafi ila anabadilishwa mwili na kuwa na nafsi hai.
[B]
Amewaingiza wengi kwenye Ibada za Umizimu bila kujua. Kuomba, Kuongea na Wafu na kuwaombea wafu ni Ibada za Umizimu, Kwa kuamini kuwa Wafu wako mbinguni, Shetani anajigeuza na kuja kwa sura za watakatifu waliokufa na kuwaagiza watu wamwabudu Mungu kwa njia ambazo zingine ni kinyume na Maandiko. Ibada ya Sanamu, Lozari na sadaka ya wafu walioko pagatori ni baadhi ya mafundisho yaliyoingizwa kanisani kwa hila ya mwovu na wengi hawajui.Kuomba au kuwaombea Wafu Ni machukizo kwa Bwana ( Kumbukumbu la torati 18:9-12 ).
[C]
Amefanikiwa kueneza Imani ya Pagatori, ambayo amewafanya mamilioni ya watu wapotee, kwa kutojiandaa wakiwa Hai, wakitegemea kuja Kuombewa na kutolewa sadaka ya msamaha na ndugu zao walio hai ili watoke Pagatori na kwenda peponi.
[D]
Amewafanya wengi wachanganyikiwe wasielewe sawasawa Ahadi za Kristo juu ya Kurudi mara ya pili kuja kuuhukumu ulimwengu, na Injili kuhusu Kiama imevurugwa. Pia amewaminisha wengi kuwa Mungu si wa HAKI kwani anawapeleka Jehanamu kabla ya, Hukumu na wenye Mapesa wanaweza kumlipa wakasamehewa wakiwa pagatori, hivyo kumfanya Mungu kuwa anaupendeleo.
Ndugu yangu inakupasa uchague leo kuwa katika wokovu wa kweli au wokovu ambao Kristo aliuita wa watu
wapumbavu, yaani wale wanaomkiri Kristo kuwa mwokozi wao kwa midomo tu ila wanakataa kutii Neno lake.
Yesu anakuita kwa Upole na kukutahadharisha, Fanya uamuzi sasa.
[ Mathayo 7:24-27 , Ufunuo 18:4-5 ]