Uchunguzi uliofanywa hadi sasa kuhusiana na kisanduku cheusi cha ndege ya Urusi iliyoanguka wiki iliyopita katika milima ya Sinai nchini Misri
na kuua watu wote 224 waliokuwemo ndani yake unaashiria mripuko wa bomu kuwa chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo. Hiyo ni kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyo karibu na wachunguzi wa ajali hiyo. Taarifa za awali kuhusiana na tathimini iliyokwishafanyika inaonesha kuwa ndege hiyo ilianguka baada ya bomu lililokuwa ndani yake kuripuka. Chanzo kingine kinasema kuwa ndege hiyo ilishuka na kuanguka ghafla muda mchache tu baada ya kuruka kutoka katika mji wa Sharm el-Sheikh jumamosi iliyopita.Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kwenda mji wa Saint Petersburg nchini Urusi.
Kundi la dola la kiisilamu lilidai kuhusika na kuanguka kwa ndege hiyo.Awali Urusi ilikataa kukubaliana na taarifa za kuhusishwa kwa shambulizi la aina yoyote na kuanguka kwa ndege hiyo na hadi sasa haijatoa kauli rasmi ya kukubaliana na taarifa hizo mnamo wakati ikisimamisha safari za ndege zake kwa sasa kwenda nchini Misri