Pendekezo hilo la waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere linaonekana kuwashangaza baadhi ya washirika katika serikali ya kansela Angela Merkel na kuleta mkanganyiko mwingine kuhusiana na jinsi serikali inavyolishughulikia suala la wakimbizi.
Wizara ya De Maiziere imesema wazo hilo ni kwamba Wasyria ambao hawatatoa kwa maafisa ushahidi wa kusumbuliwa binafsi lakini wanakimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa jumla watapewa, "ulinzi nusu" hali ambayo haifikii kupewa hadhi kamili ya ukimbizi lakini wanapewa watu ambao wanakabiliwa na kitisho kikubwa nchini mwao.
Wakati watu wanaopatiwa hifadhi kamili wanapata haki ya kuishi nchini Ujerumani kwa muda wa miaka mitatu, na wale wenye "ulinzi nusu" wanapata ruhusa ya ukaazi kwa mwaka mmoja ambao unaweza kurefushwa mara kadhaa.
Kuwaleta ndugu za wakimbizi
Siku ya Alhamis , Merkel na washirika wake katika serikali ya mseto walikubaliana kwamba watu wenye "hifadhi nusu" wataweza kuwaleta ndugu zao nchini Ujerumani baada ya miaka miwili.
Hawakuitaja Syria, na kwamba makubaliano hayo yanakuja pamoja na makubaliano ya kuunda vituo vipya vya kuwapokea na kushughulikia maombi yao kwa haraka zaidi kwa wale ambao hawana matumaini makubwa ya kupata hifadhi - kama wale kutoka katika mataifa ya Balkan.
De Maiziere ameiambia radio ya Ujerumani Deutschlandfunk jana Ijumaa (06.11.2015) kwamba mataifa mengine yaliyoko katika hali kama hiyo yanatoa hadhi ya ukaazi "kwa muda maalum, na sisi tutafanya hivyo katika siku za baadaye na wakimbizi kutoka Syria pia, na kwamba tunawaambia : mtapata ulinzi, lakini ni kile kinachoitwa "ulinzi wa muda."
Hakuna mabadiliko ya sera
Haikufahamika wazi ni kwa kiasi gani mhafidhina de Maiziere alijadili wazo hilo na mtu mwingine yeyote miongoni mwa washirika wa serikali ya mseto ya kansela Merkel. Ralf Stegner , mbunge kiongozi wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa shoto cha Social Democrats SPD, amesema jibu lake ni "hapana moja kwa moja."
Saa kadhaa baadaye , de Maiziere alionekana kujitoa kutoka katika pendekezo lake hilo. "Hakuna mabadiliko katika utendaji ulioidhinishwa kwa ajili ya wakimbizi wa Syria," amesema , na kuongeza kwamba mabadiliko yalipangwa mwanzoni mwa wiki.
Hata hivyo amesema , kutokana na uamuzi wa Alhamis wa kuzuwia uwezo wa baadhi ya watu kuwaleta ndugu zao nchini Ujerumani, "kuna haja ya majadiliano katika muungano wa serikali, na kwamba mambo yatabaki kwa hivi sasa kama yalivyo hadi pale uamuzi mpya utakapochukuliwa.
Wakati huo huo serikali ya Ujerumani imetoa uhakikisho jana Ijumaa (06.11.2015) kwamba hakuna mabadiliko katika sera yake ya wakimbizi wa Syria, baada ya waziri de Maiziere kusema watapatiwa hadhi pungufu ambayo inawakataza kuwaleta ndugu zao.