Ufaransa pamoja na Ubelgiji zimeanzisha msako mkali kuwatafuta watu waliohusika katika
mashambulizi ya Ijumaa usiku yaliyotokea mjini Paris na kuwaua watu 129. Msako huo ni katika juhudi za kuwatambua washambuliaji hao pamoja na watuhumiwa wakuu. Tayari orodha ya majina ya watu saba waliokufa yameshatambuliwa akiwemo mshukiwa wa kwanza, Ismail Omar Mostefai, mwenye umri wa miaka 29, aliyelipua katika ukumbi wa tamasha wa Bataclan. Mostefei ni Mfaransa mwenye asili ya Algeria. Pia, yamepatikana majina mengine ya watu ambao bado wanachunguzwa. Wakati huo huo, kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS, leo limetoa mkanda wa video unaotishia mashambulizi zaidi dhidi ya nchi zinazofanya mashambulizi dhidi yake nchini Syria na Iraq, zikiwemo Marekani na Ufaransa. Mkanda huo wa video wa dakika 11, umewaonyesha wapiganaji kadhaa wa IS, wakieleza kuwa nchi zinazoendesha operesheni dhidi ya IS zitashambuliwa kama ilivyokuwa kwa Ufaransa.