Wakati wanafunzi wa kidato cha pili wakianza mitihani jana, Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza kwamba wanafunzi watakaofeli mtihani huo hawatorudia darasa, bali wataandaliwa utaratibu maalumu wa masomo ya jioni ili kuwawezesha kitaaluma.
Utaratibu huo mpya uliotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, unafuta rasmi utaratibu wa awali ambao Serikali iliwataka wanafunzi wanaofeli mtihani huo kukariri darasa wakishindwa kufikisha wastani wa alama 30.
Dk Msonde alisema utaratibu huo mpya utawahusu pia wanafunzi wa darasa la nne ambao nao hawatalazimika kurudia darasa, bali watakuwa na muda wao wa ziada wa kusoma.
“Lengo la kuweka utaratibu huo ni kusimamia kwa karibu viwango vya ufundishaji. Wanafunzi wanaofanya vibaya wanahitaji ukaribu wa walimu na siyo kuwarudisha darasa tu,” alisema.
Akizungumzia mtihani huo ulioanza jana, alisema watahiniwa 397,250 walisajiliwa nchi nzima, wakiwamo wanafunzi 67 wasioona na 224 wenye uoni hafifu.
Mwaka 2008, Serikali ilifuta makali ya mtihani wa kidato cha pili, hali iliyotoa fursa kwa wanafunzi wengi hata wasio na uwezo kuingia kidato cha tatu na hatimaye kupata nafasi ya kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne.
Baada ya matokeo mabaya yaliyotokana na uamuzi huo na pia kelele za wadau wa elimu na jamii kwa jumla, hatimaye mwaka 2012, Serikali iliurudisha mtihani huo na kutangaza kuwa wanaofeli watakariri darasa, utaratibu ambao sasa umefutwa.