MJUE SANA MUNGU,ILI UWE NA AMANI, NDIVYO MEMA YATAKAVYOKUIJIA

Je unajitambua? by charles shibita


Jitambue by Colin MtitaJitambue by Colin Mtita

Binadamu ni viumbe wenye utashi mkubwa unaotupa uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi
 juu ya maisha yetu ya kila siku. Maamuzi husababisha maisha kusonga mbele au kurudi nyuma. Maamuzi hutokana na tabia. Tabia hujengwa kutokana na fikra na mtazamo ulionao juu ya maisha.

Tabia ni kitu kinachojijenga kwa muda mrefu kutokana na mazingira, jamii inayokuzunguka, mila na desturi, uzoefu maishani na mengineyo. Lakini tabia hutegemea zaidi fikra. Fikra potovu huleta tabia na mtazamo mbovu juu ya maisha.
Kwa ufupi ni kuwa, fikra zako ndio maisha yako. Kubadilisha maisha huanzia kwenye kujenga fikra bora. Njia pekee ya kujenga fikra na mtazamo bora wa maisha yako ni kujitambua.
Kujitambua ni swala la msingi kwa mtu yeyote mwenye nia ya kusonga mbele kimaisha au kubadilisha kabisa muelekeo wa maisha yake. Mafanikio ya kudumu huja baada ya kujitambua.
Kujitambua kunaambatana na mambo mengi ya msingi, yakiwemo – mabadiliko ya fikra, mwenendo, maamuzi na malengo ya maisha.
Kwa mtu yeyote yule, katika umri wowote ule, kujitambua ndio mwanzo wa maisha bora. Huu ndio muda muafaka wa kubadilisha muelekeo wa maisha yako.

Umuhimu wa kujitambua

Kuna faida nyingi sana zinazotokana na kujitambua, chache kati yake ni hizi :

1. Kuishi maisha yaliyo kamili

Kujitambua kunakupa nafasi ya kupanga malengo kutokana na ndoto zako maishani. Malengo ndio msingi wa maendeleo. Tatizo ni kuwa wengi wetutumejawa na hofu, kutojiamini, kuiga, kutojua cha kufanya na kutofahamu umuhimu wa fikra zetu kwenye maisha ya kila siku. Kujitambua kunakupa ujasiri wa kupambana na vikwazo katika safari ya kutimiza ndoto zako.
Kwa ufupi, kujitambua ni mwanzo wa kuishi maisha yaliyo kamili, kifikra na kimtazamo. Unaweza kufanya mambo mengi bila kujitambua, lakini mafanikio yanayodumu hayaji kwa kubahatisha, bali kwa kuelewa njia madhubuti za kufanya mambo ili uweze kufikia malengo. Hii inawezekana kwa kuanza kujitambua.

2. Kutumia kila fursa ipasavyo

Fursa ziko kila sehemu, unachohitaji ni malengo madhubuti unayotaka kutimiza. Una utashi mkubwa na vipaji vingi vinavyoweza kutumika katika kutumia fursa mbalimbali na kuinua maisha yako. Njia pekee ya kuanza kufahamu uwezo wako mkubwa ni kujitambua. Kujitambua ni kufahamu fursa unazotaka kuzitumia kuendeleza maisha kwa kufanya yale  muhimu na kuacha yasiyo na tija kwako.

3. Kujiendeleza zaidi kifikra

Fikra zako zina mchango mkubwa sana katika kuendesha maisha yako. Ili kubadili maisha, ni lazima kubadili fikra. Kubadili fikra ni kitu cha kwanza na cha msingi.
Ili tuweze kufikia malengo, tunatakiwa kupanua wigo wa fikra zetu na kuona mbali zaidi ya leo na kesho. Hii inawezekana kwa kila mmoja wetu, ingawa si kazi rahisi.

4. Kuwa mchango mkubwa kwa jamii

Binafsi naamini – maisha huwa na maana zaidi kama kile unachofanya kitakuwa na mchango mkubwa kwa watu wengi zaidi.
Mtu anayejitambua huwa rasilimali muhimu kwa jamii. Mchango wake huwa chachu ya mabadiliko katika maisha ya wengi. Maendeleo huletwa na watu wenye mtazamo chanya zaidi juu ya malengo yao maishani. Nawe pia unaweza kama ukianza kujitambua.
Kujitambua ni jambo muhimu sana ili kuweza kufanikiwa kwenye maisha yako. Ni chaguo lako – kuchukua nafasi na kuweza kujitambua au kuishi maisha uliyozea na kuendelea kushabikia wale wanaotimiza ndoto zao kila siku.
Karibu kwenye safari ya kujitambua.

Subscribe to receive free email updates: